Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)

Elimu Haki Wajibu

WATUMISHI IJA WAPATIWA MAFUNZO YA MASUALA YA WOSIA NA MIGOGORO YA ARDHI

Imewekwa: 28 March, 2025
WATUMISHI IJA WAPATIWA MAFUNZO YA MASUALA YA WOSIA NA MIGOGORO YA ARDHI

Watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wamepatiwa mafunzo juu ya uandishi wa wosia, taratibu za ununuzi wa  ardhi na  umuhimu wa kuwa na nyaraka za utambuzi zenye taarifa zinazowiana. 

Mafunzo hayo yameandaliwa na Kituo cha Msaada wa Kisheria cha Chuo na yameendeshwa na wanasheria wa kituo hicho ambao ni Wakili na Mhadhiri Roggers Cletus,  Wakili George Banoba pamoja na Afisa Sheria wa Chuo Wakili. Renatus Lugwisha.

Akifungua mafunzo hayo leo tarehe 28/03/2024 Chuoni Lushoto,  Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amesema kuwa ni mafunzo muhimu kwani yanawasaidia washiriki kufahamu taratibu za kisheria za masuala hayo ya wosia na ardhi ili kuepuka migogoro inayoweza kujitokeza hapo baadaye.

Pia amewashauri watumishi kuwa makini linapokuja suala la mali, kwani ni eneo lenye migogoro mikubwa sana.

"Nawashauri muwe makini sana katika masuala haya ya ardhi na wosia, linapokuja suala la mali, hiyo huwa ni vita kubwa," amesema Mhe. Dkt. Kihwelo.

Naye mratibu wa mafunzo hayo Wakili Banoba amesema kuwa wameyaandaa kutokana na uzoefu waliyoupata kwenye kampeni za msaada wa kisheria za Mama Samia zinazoendelea katika mikoa mbalimbali.  

"Mafunzo haya yanatokana na uzoefu tuliyoupata wakati tukiwa kwenye kampeni za msaada wa kisheria za Mama Samia ambapo migogoro ya ardhi na mirathi imekuwa mingi sana," amesema Wakili Banoba.

Akiwasilisha mada ya kwanza ya Msawazo wa taarifa za utambuzi,  wakili Cletus ambaye pia ni Mhadhiri msaidizi amesema kuwa wapo watu ambao wamekuwa wakikosa huduma mbalimbali katika ofisi za Serikali kutokana na taarifa zao zikiwemo za majina kutofautiana kwenye vyeti vyao.

Hiyo inatokana na watu kushindwa kuwa makini wanapokuwa wanaandika taarifa zao kwenye nyaraka na hivyo kuleta mkanganyiko wa taarifa.

Katika mada ya pili kuhusu wosia, Wakili Lugwisha amesema kuwa ni muhimu watu kuandika wosia ili kuepusha migogoro inayoweza kujitokeza kwenye familia mara baada ya kufariki dunia.

Amesema  kuwa warithi sahihi hukosa mali kutokana na kutokuwepo kwa wosia uliyoachwa na marehemu na hivyo kuishia kuhangaika.

Kwa upande wake wakili Banoba ambaye amewasilisha mada kuhusu ununuzi wa ardhi, amehimiza kufuatwa kwa taratibu za kisheria kabla ya ununuzi.

Amebainisha kuwa watu wengi wamekuwa wakinunua ardhi bila kufanya uchunguzi na kufuata sheria na hivyo kujikuta wanaingia kwenye migogoro ya ardhi.

Pia ameongeza kuwa wengine kwa kutokufuata utaratibu wamejikuta wakinunua ardhi ya kuweka makazi ilihali ardhi hiyo matumizi ni mengine na hivyo kupoteza bure fedha zake.

Katika mafunzo hayo watumishi walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali na kujibiwa.