IJA YAWAFUNDA WAANDISHI WA HABARI KUHUSU UANDISHI WA HABARI ZA MAHAKAMA

NA YUSUFU AHMADI, IJA
Kama sehemu ya kukuza uandishi sahihi wa habari za Mahakamani na wananchi kupata habari zenye ukweli na zilizo sahihi, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania, kimeendesha mafunzo kwa waandishi wa habari nchini juu ya uandishi sahihi wa habari za Mahakamani.
Mafunzo yamefanyika leo Julai 25, 2025 kwa njia ya mtandao ambapo zaidi ya waandishi wa habari 170 wameeshiriki mafunzo hayo kutoka sehemu mbalimbali nchini.
Kwenye neno la utangulizi, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Prof. Elisante Ole Gabriel amesema kuwa habari za Mahakamani ni nyeti sana, hivyo zinahitaji umakini katika uandishi wake.
Amesema kuwa makosa madogo kama ya alama tu za uandishi (punctuation marks) yanaweza kuzua taharuki kwa mhusika na jamii kwa ujumla.
Pia amewakumbusha waandishi wa habari kulinda faragha za watu kama watoto wadogo wakati wa kesi, kwa kuwa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 inakataza kuchapisha picha za mtoto.
Nao wakufunzi wa mafunzo hayo akiwemo Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambaye pia ni Mwanahabari, Bw. Alloyce Komba aligusia maeneo muhimu ambayo waandishi wa habari wanapaswa kuyazingatia wanapoandika habari za Mahakamani.
Alisema kuwa mwandishi wa habari anapaswa kufahamu muundo wa Mahakama nchini ili kufahamu majukumu ya kila Mahakama, majina yake pamoja na vyeo sahihi vya Majaji, Mahakimu na waendesha mashtaka.
"Wengi wetu tumezoa kuandika Mahakama ya Hakim Mkazi Kisutu, lakini usahihi ile ni Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, ila tumezoea kuiita ya Kisutu kutokana na Mahali ilipo," amesema Wakili Komba.
Pia ametaja vyanzo sahihi vya habari za Mahakamani kuwa ni Mahakamani penyewe, kutoka kwa Majaji, Mahakimu, Makarani, mawakili, waendesha mashtaka pamoja na washtakiwa wenyewe.
Hata hivyo amesisitiza umakini katika vyanzo hivyo kwa kubainisha kuwa kila chanzo kina mipaka yake katika kupata taarifa sahihi.
"Mtu kama karani sio Hakimu, hivyo usiende ukamuuliza kesi ilikuwaje, hapana huyu unapaswa tu kumuuliza tarehe ya kesi kujua imepangwa lini na sio vinginevyo," amesema.
Aidha amewasihi waandishi hao wa habari kutoweka maoni yao juu ya mwenendo wa kesi bali wao kazi yao ni kuripoti tu kile kilichojiri Mahakamani.
"Mahakamani eleza tu matukio (Court Proceedings), no opinioni (usitoe maoni yako)," amekumbusha.
Wakili Komba amewasisitiza waandishi wa habari kujiepusha na rushwa kwa kuwa kitendo hicho huchangia kuharibu mwenendo wa kesi na kuilisha jamii habari isio sahihi.
Kwa upande wake Afisa Habari, Elimu, Mawasiliano Mwandamizi wa Mahakama na pia mwanasheria Bw. Faustine Kapama amegusia vitu vya kuepuka kuandikwa yakiwemo majina ya watoto na picha zao, majina ya mashahidi na majina ya waathirika kwenye kesi za udhalilishaji wa kijinsia na kingono.
Pia amewakumbusha waandishi wa habari kutoingia kwenye mtego wa kuidharau Mahakama na hivyo kuingia matatizoni kwa uvaaji usiofaa, uvutaji wa sigara na utafunaji wa vyakula mbalimbali wawapo Mahakamani.