JAJI KIHWELO: WANACHUO ZINGATIENI NIDHAMU, JUHUDI NA UADILIFU ILI MFANIKIWE KITAALUMA NA KIMAISHA

Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amewasisitiza wanachuo kuzingatia nidhamu, juhudi na uadilifu ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao pamoja na mafanikio mengine katika maisha yao wawapo Chuoni na baada ya kumaliza.
Mhe. Dkt. Kihwelo ametoa nashaha hizo leo Juni 10, 2025 wakati akizungumza katika Baraza la Wanachuo (Students' Baraza) lililofanyika katika ukumbi wa Nyalali Chuoni hapo.
Amesema kuwa mtu yeyote atakae zingatia vitu hivyo vitatu, ana uhakika mkubwa wa kufanya vizuri darasani na pia kufanikiwa katika masuala mbalimbali kwani hizo ni miongoni mwa nguzo muhimu katika maisha ya mwanadamu.
"Bila juhudi huwezi kukipata kile unachokitaka, hivyo zingatieni sana juhudi katika masomo yenu ili mpate alama nzuri za ufaulu," amesema Mkuu wa Chuo.
Kuhusu nidhamu, amesema kuwa huo ni mtaji mkubwa wa maisha ya mwanadamu na nidhamu inasaidia kumtofautisha mtu mmoja na mwingine.
"Nidhamu ni mtaji wa maisha, watu wengi waliofanikiwa katika maisha yao wana nidhamu katika vipengele mbalimbali vya maisha," amesema Mhe. Dkt. Kihwelo.
Amewasisitiza kuzingatia nidhamu ya kusikiliza masomo darasani, kuwahi darasani na matumizi mazuri ya pesa.
Kwenye uadilifu, Mkuu wa Chuo amesema kuwa bila uadilifu ni vigumu kuaminiwa na watu na hivyo kupelekea kukosa fursa mbalimbali za kimaisha.
Kwa upande mwingine, Mhe. Dkt. Kihwelo amewasihi wanachuo hao kutambua kuwa lengo lao la kwanza la kuwepo hapa Chuoni ni kusoma.
"Naamini ninyi nyote mpo hapa IJA kwa ajili ya elimu, hayo mengine ni ziada tu, hivyo zingatieni sana masomo yenu, msikimbilie mambo mengine yatakayoathiri ufaulu wenu," amesema Mhe. Dkt. Kihwelo.
Aidha amewaomba wanachuo hao kukitangaza Chuo pamoja na kuwa na sifa njema wawapo nje ya Chuo.
Kwa upande wake, Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala Profesa Fatihiya Massawe amewasihi wanachuo kutojiingiza katika mambo yatakayoathiri masomo yao.
Naye Mkurugenzi wa Taalauma ambaye pia ni Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo, Taaluma, Utafiti na Ushauri Elekezi Bw. Emily Suka amesema kuwa katika kuimarisha ufaulu na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za wanachuo, Chuo kimewapatia washauri maalumu kwa ajili ya kushughulikia changamoto hizo.
Akitoa neno la shukrani, Rais wa Serikali ya wanachuo (IJASO) Bw. Robert Kinyangasi amemshukuru Mkuu wa Chuo kwa nasaha zake na kuahidi kuwa wao kama wanachuo watasoma kwa bidii na kufaulu.
Nao wanachuo wamepata nafasi ya kulezea changamoto mbalimbali zinazowakumba huku uongozi ukifafanua juhudi zilizofanyika pamoja na kushugulikia changamoto ambazo zimeibuliwa.