JAJI MKUU AHIMIZA UADILIFU NA MATUMIZI YA TEHAMA

Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim H. Juma amesema kuwa uadilifu ni muhimu katika utoaji wa haki huku akihimiza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika uendeshaji wa mashauri ili kurahisisha utendaji wa kazi ikiwa ni pamoja na kupunguza mrundikano wa mashauri hayo.
Amesema hayo wakati akifungua Mafunzo Elekezi kwa Majaji watano (5) wa Mahakama ya Rufani leo April 28, 2025 katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), wilayani Lushoto mkoani Tanga. Mafunzo haya yatakayofanyika mpaka tarehe 02/05/2025 yameandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na IJA.
“Unaweza kuwa na sheria nzuri na sheria nzuri zipo, lakini sheria nzuri haitoshi, kama mtekelezaji wa sheria hana kiini cha utoaji wa haki, na hapa sio Jaji tu, hata Mawakili, uadilifu ni kwa wote,” amesema Mhe. Prof. Juma na kuongeza,
“Haitakuwa na maana au tija kama tutakuwa na sheria halafu sheria hizo zinasimamiwa na Majaji wasiofaa na Wanasheria wasio waadilifu.”
Kwenye upande wa mwingine, Mhe. Jaji Mkuu amewahimiza Majaji hao wa Mahakama ya Rufani kuhakikisha wanatilia mkazo matumizi ya TEHAMA akisema kuwa katika ulimwengu wa sasa matumizi ya TEHAMA hayakwepeki na kwamba yana faida katika kupunguza mrundikano wa mashauri kwa Jaji kuweza kuendesha mashauri sehemu yoyote alipo.
Aidha Mhe. Prof. Juma amehimiza Majaji kujifunza akili hisia (Emotional intelligence) akisema kuwa humsaidia Jaji kubaini na kudhibiti hasira zake pamoja na zao wengine na hivyo kuepusha mikwaruzano na wenzao.
Majaji wanaopatiwa mafunzo ni aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Feleshi, Mhe. Jaji Latifa Mansoor, Mhe. Jaji George Masaju, Mhe. Jaji Dkt. Deo John Nangela, na Mhe. Jaji Prof. John Ubena.
Naye Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amesema kuwa hayo ni mafunzo ya kundi la tano la Majaji wa Mahakama ya Rufani na kubainisha kuwa yatawasaidia kuboresha utendaji wao wa kazi.
Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tanga Mhe. Katarina Mteule amempongeza Jaji Mkuu kwa kuchagiza matumizi ya mtandao katika uendeshaji wa mashauri Mahakamani akisema kuwa matumizi hayo yamesaidia kuondoa kero nyingi kwa wananchi ikiwemo kupunguza gharama za usafiri na za malazi.
Ametolea mfano wa jinsi matumizi ya mtandao yanavyowasaidia wananchi wa wilaya ya Kilindi ambao huzifuata huduma za Mahakama Kuu jijini Tanga umbali wa kilomita zaidi ya 210, akisema kuwa kwa sasa wengi wao hawalazimika kwenda Tanga kwani mashauri yao husikilizwa wakiwa huko huko wilayani kwao.
Ufunguzi huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya na viongozi wengine wa Mahakama.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya mafunzo ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2013, Mpango mkakati wa Mahakama ya Tanzania 2021/22-2024/25, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja na Mpango Mkakati wa IJA wa mwaka 2023/24-2027/28.