Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)

Elimu Haki Wajibu

MAJAJI NA MAHAKIMU WASHIRIKI MAFUNZO YA UTATUZI WA MIGOGORO KWA NJIA YA USULUHISHI

Imewekwa: 22 July, 2025
MAJAJI NA MAHAKIMU WASHIRIKI MAFUNZO YA UTATUZI WA MIGOGORO KWA NJIA YA USULUHISHI

Katika jitihada za kukuza mbinu mbadala za utatuzi wa migogoro na kuongeza ufanisi katika mifumo ya utoaji haki hapa nchini, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Majaji kutoka Ujerumani kwa ufadhili wa Shirika la Ushirikiano wa Kimataifa la Ujerumani (GIZ), wanaendesha mafunzo ya usuluhishi kwa njia mbadala kwa Mafisa wa Mahakama ya Tanzania.

Mafunzo hayo ya wiki moja yanalenga pia kubadilishana uzoefu baina ya Majaji wa Tanzania na  Ujerumani, pamoja na kukuza matumizi ya usuluhishi hapa nchini.

Akifungua mafunzo hayo katika Hoteli ya Slipway mkoani Dar es Salaam  Julai 21, 2025, Jaji wa Mahakama ya Rufani ambaye pia ni Mkuu wa Chuo Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amesema kuwa usuluhishi ni chombo muhimu katika kuimarisha upatikanaji wa haki, kulinda mahusiano ya kijamii, na kupunguza mzigo wa mashauri kwenye mfumo rasmi wa Mahakama. 

“Ni ukweli ulio wazi kwamba, usuluhishi sio tu njia mbadala, bali pia ni nyenzo ya msingi katika kutoa haki kwa haraka, kuendeleza uhusiano na kupunguza mrundikao wa mashauri Mahakamani,” amesema Mhe. Dkt. Kihwelo.

Ameongeza kuwa mafunzo haya yanasaidia kuwapatia washiriki mbinu na ujuzi wa kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi. 

Chimbuko la  mafunzo haya ni ziara iliyofanywa na maafisa wa Mahakama  nchini Ujerumani Novemba 2024 ambapo walijifunza namna ambavyo mfumo wa sheria nchini Ujerumani unavyotumia njia za usuluhishi kwa mafanikio makubwa.

Kwa upande mwingine, Mhe. Dkt. Kihwelo ameishukuru na kuipongeza  GIZ  kwa ushirikiano wake madhubuti katika kuandaa nyenzo za mafunzo na shughuli nyingine za kuimarisha mifumo ya utoaji haki hapa nchini.

Naye Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani nchini Ujerumani ambaye pia ni mratibu wa zamani wa masuala ya usuluhishi wa kimahakama katika mji wa Berlin Mhe. Anne-Ruth Moltmann-Willisch, amesema kuwa  mafunzo haya yatasaidia kuimarisha mifumo ya utoaji haki kwa Tanzania na Ujerumani kupitia njia za usuluhishi.

Kwa upande wake Meneja Mradi wa Upatikanaji wa haki kwa jamii ya Wanawake na watoto (SAFE) hapa Tanzania Bi. Katharina Kuehn ambaye alitoa neno la utangulizi amebainisha kuwa hakuna njia moja za kuendesha usuluhishi kwa kuwa mfumo huo unategemea na mbinu za kila mmoja.

“Hakuna mtindo mmoja wa kuendesha usuluhishi hapa duniani, kama ilivyo kwa sheria zingine, hivyo kila mmoja wetu hapa kupitia uzoefu wake atasaidia sisi sote kuweza kujifunza mbinu bora za kufanya usuluhishi,” amesema Bi. Kuehn.

Vilevile mafunzo haya yatafuatiwa na mafunzo ya wakufunzi kwa ajili ya kuwajengea uwezo baadhi ya washiriki ambao nao wataenda kuwafundisha wengine.

IJA na GIZ wamekuwa wakishirikiana katika maeneo mbalimbali ambapo Juni mwaka jana waliendesha mafunzo yanayohusu Kanuni za Maadili ya Kimahakama (Bangalore Principles) kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Septemba mwaka jana walishrikiana kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa wakazi wa kata za Mbaramo na Mnazi wilayani Lushoto.