Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)

Elimu Haki Wajibu

MAFUNZO YA UTAFITI WA KISHERIA YATOLEWA KWA MAJAJI NA MAHAKIMU

Imewekwa: 05 August, 2025
MAFUNZO YA  UTAFITI WA KISHERIA YATOLEWA KWA MAJAJI NA MAHAKIMU

Katika jitihada za kuimarisha  utafiti wa kisheria na kuwezesha utoaji bora wa maamuzi ya Kimahakama, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Taasisi ya  Laws.Africa, AfricaLII na Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Ujerumani ( GIZ) zimeendesha mafunzo ya wakufunzi (Training of the Trainers) ya utafiti wa kisheria kwa Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Naibu Wasajili na Mahakimu Wakazi.

Mafunzo hayo yamefunguliwa  na Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo Agosti 04, 2025 na yanafanyika katika Hoteli ya Four Points jijini Dar es Salaam.

Lengo kuu ni kuboresha uwezo wa washiriki katika utafiti wa kisheria na kuwaandaa kuwa wakufunzi kwa wenzao.

Katika hotuba yake, Mhe. Dkt. Kihwelo amesema kuwa utafiti wa kisheria ni nyenzo muhimu katika utoaji wa maamuzi ya Kimahakama nani nguzo katika utawala wa sheria.

Pia aliongeza kuwa maamuzi yanayotolewa ni muhimu yakajengwa katika utafiti wa kina, na kwamba uamuzi mzuri ni ule uliyofanyiwa utafiti.

“Maamuzi yetu lazima yajengwe juu ya utafiti wa kina, na usiobebwa na hisia za  upendeleo. Uamuzi uliofanyiwa utafiti mzuri na kuandikwa kwa weledi hujenga uaminifu kwa umma, imani ni muhimu pia kwa Mahakama,” alisisitiza.

Pia alibainisha kuwa utafiti wa kisheria hauishii tu katika kutafuta kesi au sheria, bali unahusisha uchambuzi yakinifu wa vyanzo vya sheria na matumizi sahihi katika mazingira husika ili kutoa maamuzi yenye msingi thabiti.

Aidha alitoa shukrani zake za dhati kwa Taasisi ya Kimataifa ya  Laws.Africa, AfricaLII kwa kushiriki kuandaa mafunzo pamoja na Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Ujerumani ( GIZ) kwa ufadhili wa mafunzo hayo.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Biashara Mhe. Dkt. Mwajuma Kadilu ambaye pia ni mwezeshaji wa mafunzo hayo, pamoja na wawakilishi kutoka GIZ Tanzania akiwemo Bw. Muhamet Brahimi, Meneja Mradi wa Ukuzaji wa Utawala wa Sheria na Mahakama Barani Afrika (ProLA).