Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)

Elimu Haki Wajibu

MKUU WA WILAYA YA LUSHOTO AAHIDI USHIRIKIANO NA IJA KUTOA ELIMU NA MSAADA WA KISHERIA KWA JAMII

Imewekwa: 02 May, 2025
MKUU WA WILAYA YA LUSHOTO AAHIDI USHIRIKIANO NA IJA KUTOA ELIMU NA MSAADA WA KISHERIA KWA JAMII

Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Mhe. Zephania Sumaye ameunga mkono mpango kazi wa Kituo cha Msaada wa Kisheria cha Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wa kutoa elimu na msaada wa kisheria kwa jamii ya Lushoto.

Mkuu huyo wa Wilaya ametoa ahadi hiyo alipokutana na timu ya Kituo hicho cha Msaada wa Kisheria ofisini kwake leo Mei 02, 2025.

Timu hiyo iliyongozwa na Mratibu wa kituo hicho Bi. Jackline Kulwa imefika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya kwa ajili ya kuwasilisha Mpango Kazi wa utoaji wa elimu na msaada wa kisheria katika maeneo mbalimbali ya Lushoto.

Akiongea na timu hiyo, Mhe. Sumaye ameipongeza kwa kuja na mpango kazi huo na kwamba yupo tayari kushirikiana nayo ili kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za kisheria zinazoikabili jamii ya Lushoto.

"Hili mnalotaka kulifanya ni jambo jema sana, nami kama Mkuu wa Wilaya nalibariki na tutashirikiana katika kampeni hii ili tuwasaidie wananchi wetu katika changamoto hizi za kisheria," amesema Mhe. Sumaye. 

Pia ameongeza kuwa kampeni hizo ni muhimu kwani zitakisaidia Chuo kujitangaza (publicity) kwa jamii ya Lushoto na nchi kwa ujumla.

Awali mratibu wa kituo hicho ambaye pia ni Afisa Sheria wa Chuo Bi. Jackline Kulwa ameeleza kuwa kituo hicho kimepanga kutembelea maeneo mbalimbali ya Lushoto ili kutoa elimu na msaada wa kisheria katika vipengele vya mirathi, migogoro ya ardhi, ndoa na masuala ya ukatili wa kijinsia.

Wengine waliyokuwepo kwenye timu hiyo ni Mhadhiri Msaidizi wa Chuo, Bw. Roggers Cletus, Mlezi wa Wananchuo, wakili George Banoba, Msaidizi wa kisheria, Bi. Diana Godfrey, Mlezi wa Wanachuo Bw. Joshua Senguo.

Aidha timu hiyo imefika ofisini kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto na kukutana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji Bw. Rogath C. Nlulu.

Bw. Nlulu amefurahishwa na mpango huo na kusema kuwa ofisi yake itawezesha kampeni hiyo ifanyike kwa ufanisi.

Kituo cha msaada wa kisheria cha Chuo kimekuwa kikitoa elimu na msaada wa kisheria kwa jamii mbalimbali ambapo Novemba mwaka jana kilitoa Elimu ya Utatuzi wa Migogoro kwa njia ya Usuluhishi katika Mahakama ya Mwanzo Soni Wilayani Lushoto.

Pia Septemba mwaka jana kilishirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) pamoja na Asasi ya kiraia ya Legal Vision Organisation (LEVO) kutoa elimu kwa wakazi wa kata za Mbaramo na Mnazi Wilayani Lushoto.

Aidha timu ya kituo hicho imeshiriki katika Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia(MSLAC) zinazofanyika maeneo mbalimbali nchini.