Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)

Elimu Haki Wajibu

PROF. FATIHIYA AWASHAURI IJASO KUACHA ALAMA KWENYE UONGOZI WAO

Imewekwa: 09 April, 2025
PROF. FATIHIYA AWASHAURI IJASO KUACHA ALAMA KWENYE UONGOZI WAO

Naibu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mipango, Fedha na Utawala Prof. Fatihiya Massawe amewahimiza viongozi wa Serikali ya Wanachuo (IJASO) kwa *mwaka wa masomo 20* *24/2025* kuhakikisha wanafanya mambo makubwa na yenye tija ili waache alama kwenye uongozi wao.

Prof. Fatihiya ametoa nasaha hizo leo Jumatano tarehe 09/04/2025 Chuoni Lushoto wakati akizungumza na viongozi hao  kuhusu masuala mbalimbali ya Uongozi, nidhamu na ya Chuo kwa ujumla.

"Kwa nafasi yenu ya  viongozi wa IJASO, hakikisheni  mnapanga mipango ya utekelezaji wa shughuli za Serikali ya Wanachuo ambayo itakuwa na tija kwa Serikali yenu, Chuo na kuacha  alama," amesema Prof. Fatihiya.

Pia Naibu huyo amewakumbusha viongozi hao kuwa IJASO ni chombo kikubwa hivyo wanapaswa kukitendea haki kwa kufanya kazi kwa bidii, ufanisi na uadilifu ili waweze kuwatumikia vema wapiga kura wao.

Vilevile amewataka viongozi hao kuwaheshimu watendaji mbalimbali waliyopo Chuoni pamoja na kuwa na tabia njema na mwenendo mzuri kwa jamii ili wanapomaliza Chuo wawe na sifa njema huko waendako.

Vilevile amewataka wahakikishe wanatunza miundombinu na mali za Chuo pamoja na matumizi sahihi ya huduma mbalimbali zikiwemo za maji na umeme ili kuepusha gharama kubwa za huduma hizo.

Aidha katika kikao hicho, Mwanasheria wa Chuo, Bi. Jackline Kulwa amewapitisha Wanachuo hao katika kuzifahamu kanuni za Chuo zinazowasimamia  na kuainisha kwa ufupi makosa mbalimbali ambayo wanachuo wanapaswa kuyaepuka ikiwemo kusimamishwa masomo.

Katika kikao wanachuo wamewasilisha changamoto mbalimbali zinawakabili, ambazo zimejibiwa na Prof. Fatihiya.

Aidha, Watumishi mbalimbali wa Chuo wamehudhuria kikao hicho akiwemo Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Wanachuo Bi. Frida Nicholaus, Walezi Bw. Joshua Senguo, Bw. Rajabu Mussa, Bi. Hildagarda Mushi na Rais wa IJASO Bw. Robert Kinyangasi.