STUDIO YA MAFUNZO MTANDAONI IJA MBIONI KUKAMILIKA

Studio mpya na ya kisasa kwa ajili ya kuandaa na kuzalisha maudhui mbalimbali yakiwemo ya kutoa mafunzo kwa njia ya mtandao (e-learning training) iliyojengwa katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) ipo mbioni kukamilika baada ya kufikia hatua ya ufungaji wa vifaa vya kuendeshea vipindi na kuzalisha maudhui hayo.
Studio hiyo ambayo usanifu wake ulianza Februari mwaka 2024 itakuwa ikizalisha vipindi vya maudhui mbalimbali yakiwemo mafunzo ya Kimahakama kwa ajili ya Watumishi wa Mahakama kujisomea pamoja na vipindi vingine vya sheria ambavyo vitakuwa vinarushwa mtandaoni.
Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo ametembelea studio hiyo Agosti 18, 2025 ili kujionea zoezi la ufungaji wa vifaa hivyo pamoja na kufanya majaribio ya vifaa hivyo.
Akizungumzia hatua hiyo, Mhe. Dkt. Kihwelo ameelezea kufarijika kwake na hatua iliyofikiwa ya kufunga vifaa ili matumizi rasmi ya studio hiyo yaanze na hivyo kuleta tija iliyokusudiwa.
“Binafsi nimefarijika sana kutembelea studio hii nakuona kile kinachoendelea, studio hizi zinaakisi kile ambacho tumekuwa tunakisema juu ya Mahakama na IJA kuwa na mifumo ya kidigitali katika kutoa huduma mbalimbali za Kimahakama pamoja na mafunzo” amesema Mhe. Dkt. Kihwelo.
Pia ameongeza; “ Studio hizi ni fahari kwetu na ni ndoto ambayo kwa sasa inatimia.”
Aidha amewapongeza viongozi wakuu wa Mahakama na watumishi wengine kwa jitihada na dhamira zao za dhati za kutekeleza mradi huo ambao umebeba faida kubwa kwa Mahakama, IJA na jamii kwa ujumla.
Studio hiyo imejengwa na Mahakama ya Tanzania kwa ufadhili wa Serikali kupitia mkopo wa Benki ya Dunia na ni sehemu ya maboresho ya Mahakama ya kuelekea Mahakama Mtandao katika jitihada za kutimiza ndoto ya Tanzania ya Kidigitali.