Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)

Elimu Haki Wajibu

WANAWAKE IJA WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI NA KUHIMIZA ELIMU YA SHERIA

Imewekwa: 09 March, 2025
WANAWAKE  IJA WAADHIMISHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI NA KUHIMIZA ELIMU YA SHERIA

Watumishi wanawake wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wameungana na wanawake wenzao duniani katika kuadhimisha kilele cha Siku ya Wanawake duniani jana tarehe 08/03/2025 na kusisitiza umuhimu wa watoto kupatiwa elimu ya sheria ili iwasaidie katika masuala mbalimbali yakiwemo ya ukatili wa kijinsia.

Madhimisho ya mwaka huu  yamefanyika katika kata ya Mlola iliyopo wilayani Lushoto mkoani Tanga na yamehudhuriwa na Watumishi mbalimbali wakiwemo wa Mahakama ya wilaya ya Lushoto, Taasisi mbalimbali za Serikali, Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Jeshi la Polsi, Asasi za kiraia, wanafunzi wa Shule za Sekondari na Msingi pamoja na wakazi wa eneo hilo.

Ngoma za asili ya kisambaa, mchezo wa mpira wa miguu kwa wanawake, kukimbiza kuku, kuvuta kamba, mbio za magunia na onesho la burudani ya Muziki ni miongoni mwa vitu vilivyopamba maadhimisho ya kiwilaya.

Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa wilaya ya Lushoto Mhe. Zephania Sumaye ambaye ameiasa jamii kuachana na  mila zinazokwamisha usawa wa kijinsia na kuviza maendeleo ya mwanamke.

Pia ameiasa jamii kuhakikisha mapambano ya kupigania usawa wa kijinsia yanawajumuisha wanawake na wanaume ili jinsi moja isiachwe sana nyuma. 

Akitoa salamu za IJA, Naibu Mkuu wa Chuo, Mipango, Fedha na Utawala Prof. Fatihiya Massawe kuwa Chuo kinachangia moja kwa moja kwenye kaulimbiu ya mwaka huu kwani kimejikita katika kujenga uwezo wa wataalamu wa utoaji haki kwa kutoa mafunzo ya Astashahada na Stashahada ya Sheria.

Kutokana na hali hiyo, amewahimiza wazazi na walezi wenye watoto waliyomaliza kidato cha nne mwaka 2024 kuwaleta watoto wao kupata elimu hiyo ili wakawe chachu katika kuwasaidia wazazi, walezi, jamii na taifa kwa ujumla.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya mwanamke duniani mwaka huu 2025 ni  "Wanawake na Wasichana: Tuimarishe Haki, Usawa na Uwezeshaji."