WASHIRIKI 36 KIGOMA, SONGEA WAANZA KUPATIWA MAFUNZO YA KUEPUKA KUTONESHA MAJERAHA KWA WAATHIRIKA WA UKATILI WA KINGONO

Na Aidan Robert-Mahakama Kigoma
Washiriki 36 katika mikoa ya Kigoma (18) na Songea (18) ambao ni Mahakimu Wakazi, Waendesha Mashtaka, na Maafisa Ustawi wa Jamii wameanza kupatiwa mafunzo maalumu ya kuepuka kutonesha majeraha kwa Waathirika wa Ukatili wa Kingono( Avoiding Re-traumatization to sexual abuse victims) wakati wa utoaji wa ushahidi Mahakamani.
Mafunzo hayo yamefunguliwa kwa pamoja leo Juni 24, 2025 ambapo huko mkoani Kigoma yamefunguliwa na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji John Nkwabi, na huko Songea yamefunguliwa na Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea Mhe. James Karayemaha.
Aidha mafunzo hayo ya siku tatu ambayo ni ya awamu ya nne yameandaliwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Irish Rule of Law International (IRLI) kupitia ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania.
Katika hotuba yake, Mhe. Jaji Nkwabi amesisitiza umuhimu wa lugha ya stara, huruma kwa waathirika wa ukatili wa kingono kabla, wakati wa uendeshaji wa mashauri ya makosa ya vitendo hivyo.
“Ni muhimu kutumia lugha yenye huruma, staha na weledi mkubwa, pamoja na kujenga mazingira ya kimahakama yenye usalama kwa waathirika wa ukatili huo wa kingono,” amesema Mhe. Nkwabi.
Vilevile, amehimiza washiriki kuwa makini na mbinu wanazotumia katika kushughulikia mashahidi walio katika mazingira magumu ili wasiwajengee hali ya woga au kukumbuka majeraha yao ya awali na hivyo kushindwa kutoa ushahidi vizuri.
Nao waratibu wa mafunzo hayo Mhe. Gloria Shuma katika mkoa wa Kigoma na Mhe. Patrick Lipiki huko mkoani Ruvuma wamesema kuwa katika mafunzo hayo, washiriki watapata fursa ya kujadili matukio halisi, kushiriki mazoezi ya vitendo, na kuibua maeneo yanayohitaji maboresho ya kitaasisi.
Awamu nyingine za mafunzo ya aina hii zimeshafanyika katika mikoa ya Tanga, hususani Wilayani Lushoto, Dodoma na Dar es Salaam.
Mafunzo haya yamekuwa sehemu ya jitihada za Mahakama ya Tanzania za kuboresha mifumo ya utoaji haki ili iwe jumuishi, yenye huruma, na inayowajali wahitaji wa huduma za haki hasa kutoka makundi yaliyo hatarini.