Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)

Elimu Haki Wajibu

WATUMISHI IJA WAADHIMISHA MEI MOSI, WAMUAGA MWENZAO

Imewekwa: 01 May, 2025
WATUMISHI IJA WAADHIMISHA MEI MOSI, WAMUAGA MWENZAO

Watumishi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wameadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani leo Mei 1, 2025 hapa Chuoni Lushoto kwa kufanya sherehe iliyokuwa na matukio mbalimbali.

Matukio hayo ni kumpongeza na kumuaga Bw. Shaban Ramadhani ambaye amestaafu kwa mujibu wa sheria baada ya kukitumikia Chuo kwa miaka 30.

Mzee Shaban ameagwa kwa kutunukiwa Cheti cha shukrani, ngao na zawadi zingine kutoka kwa Watumishi pamoja na zawadi kutoka kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani waliyopo kwenye mafunzo elekezi hapa Chuoni.

Matukio mengine yalikuwa ni kutoa zawadi kwa Mfanyakazi bora wa Chuo kwa mwaka 2024/2025, Afisa Rasilimaliwatu Bw. Prayson Kimaro ambaye ametunukiwa Cheti cha pongezi, na fedha.

Wafanyakazi wengine waliyopongezwa na kutunukiwa zawadi mbalimbali ni Afisa udahili Bi. Magdalena Mlumbe, Dereva Bw. Mustafa Magembe na Mhadhiri msaidizi Bi. Rose Jally ambao wamekuwa wafanyakazi hodari.

Akitoa nasaha zake, Mkuu wa Chuo ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani. Mhe. Dkt. Paul F. Kihwelo amewasihi watumishi kufanya kazi kwa bidii, weledi na uadilifu.

"Tufanye kazi kwa bidii, weledi na uadilifu, changamoto zipo ila zisitufanye tushindwe kutekeleza majukumu yetu," amesema Mhe. Dkt. Kihwelo.

Vilevile amempongeza Bw. Shaban kwa kumaliza salama muda wake wa utumishi wa umma pamoja na kumpongeza mfanyakazi bora na hodari.

Naye Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Latifa Mansoor ambaye amehudhuria sherehe hizo amewashauri watumishi kuhakikisha wanafanya kazi sana ila wasisahau kujipa muda wa kufurahi na kuburudika.

Awali, akisoma risala kwa niaba ya Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Ufundi Stadi, Ushauri na Utafiti (RAAWU) Tawi la Chuo Bw. Daniel.D. Lusa ameushukuru uongozi wa Chuo kwa kuwa na uhusiano mzuri na chama hicho.

Akisoma wasifu wa Bw. Shaban, Meneja Rasilimaliwatu na Utawala, Bw. Halid Magenda amemtaja kuwa alikuwa na nidhamu na uadilifu katika kipindi chake cha utumishi.

Kwa upande wake Mstaafu Bw. Shaban amewashukuru watumishi wa IJA kwa zawadi mbalimbali walizompatia na kuwahimiza waendelee kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kutokuchoka.