Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA)

Elimu Haki Wajibu

WIZARA YA MALIASILI, IJA NA LEAT WAJADILI MIKAKATI YA USIMAMIZI WA MISITU

Imewekwa: 18 June, 2025
WIZARA YA MALIASILI, IJA NA LEAT WAJADILI MIKAKATI YA USIMAMIZI WA MISITU

Maafisa kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) pamoja na wa Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT) wamekutana leo Juni 18, 2025 na kujadiliana juu ya namna ya utekelezaji wa mradi unaolenga kuhifadhi rasilimali za misitu ili kukabiliana na athari za uharibifu wa misitu hiyo.

Maafisa hao wamekutana  Chuoni Lushoto ambapo wamejadili mradi huo wa Mbinu Jumuishi za kuboresha Mnyororo wa Thamani wa Nishati ya Miti (Integrated Approach for Transformation of Tanzania fuel wood value chain) ambao unalenga kuimarisha uwezo wa Taasisi za Serikali na wadau wengine katika usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu ili kuzalisha nishati itokanayo na miti bila kuathiri mazingira.

Akizungumzia mradi huo, Afisa kiungo wa mradi (Focal person) ambaye pia ni Naibu Mkuu wa Chuo Mipango, Fedha na Utawala wa Chuo cha Misitu  cha Olmotonyi Dr. Angelingis Makata amesema kuwa umetokana na utafiti unaonesha kuwepo kwa pengo (gap) katika kusimamia sheria, kanuni na miongozo inayohusu ulinzi wa rasilimali za misitu na Wanyamapori kutoka kwa Taasisi zinazowajibika na usimamizi wa rasilimali hizo.

Hivyo amesema kuwa mradi huo unalenga kuimarisha eneo hilo kwa kutoa mafunzo, elimu kwa Taasisi za Serikali, Vyuo na Mamlaka  mbalimbali zinazosimamia sheria na kanuni za usimamizi wa misitu hiyo hapa nchini.

Naye mratibu wa mradi huo kutoka LEAT Wakili. Rajab H. Rajab amesema kuwa wamekuja Chuoni ili kujadili juu ya namna Chuo kitavyoweza kutoa mafunzo maalumu ya usimamizi wa sheria na miongozo hiyo ya misitu kwa Maafisa wa Mahakama na wadau wengine.

Ameongeza kuwa mradi huo unaofadhiliwa na Jumuiya ya Umoja wa Ulaya unatekelezwa katika Halmashauri za Wilaya 17.

Awali, Naibu Mkuu wa Chuo, Mipango, Fedha na Utawala Prof. Fatihiya Massawe aliwaeleza Maafsa hao kuwa Chuo kina uzoefu wa miaka mingi wa kuendesha miradi ya aina hiyo kwa kuwa kimekuwa kikitoa mafunzo kwa Mahakimu, Waendesha Mashtaka na Wapelelezi, maafisa wa Polisi juu ya namna bora ya uendeshaji wa mashauri ya wanyamapori na misitu.

“Hapa mpo eneo sahihi kwani Chuo kina uzoefu mkubwa wa kutoa mafunzo kwa wadau wa mnyororo wa utoaji haki katika kusimamia utekelezaji wa sheria. Chuo kimefanya kazi na wadau wa ndani na nje ya nchi katika sekta ya maliasili na utunzaji wa mazingira,” amesema Prof. Fatihiya.

Pia ameongeza: “ Chuo kina mbinu ya kipekee ya kuwakutanisha wadau muhimu katika mnyororo wa utoaji haki wakiwemo maafisa wa Mahakama, wapelelezi na waendesha Mashtaka.”

Maafisa wengine waliyohudhuria kikao hicho ni Katibu wa Mkuu wa Chuo, Mhe. Patrick Lipiki, Mratibu wa Mafunzo-Kurugenzi ya Mafunzo Endelevu ya Kimahakama IJA, Wakili Renatus Lugwisha na Afisa Ufuatiliaji na Tathmini wa LEAT, B. Mary Joseph Kessy.